Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Ali Al-Khatib, Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Waislamu wa Kishia wa Lebanon, alimlaki Papa Laon wa Kumi na Nne kwa niaba ya “Baraza Kuu la Kiislamu la Waislamu wa Kishia” na kwa niaba ya Waislamu wa Kishia kwa ujumla. Akimhutubia, alisema:
Tunakushukuru kwa kuitembelea nchi yetu, na tunathamini misimamo yako katika kipindi hiki kigumu ambacho taifa letu linakipitia. Tunakukaribisha kwa salamu ya Kiislamu inayoamini kuwa Nabii Isa (a.s) kama Mtume, Nabii, mtoa bishara na mwongozi.
Katika mazungumzo ya maelewano kati ya dini mbalimbali ambayo yalifanyika katika Uwanja wa Mashahidi katikati ya mji wa Beirut, kwa ushiriki wa Papa Laon, Sheikh Al-Khatib alisema: Salamu nyingi kwako kutoka Lebanon iliyojeruhiwa ambayo kiti cha Uaskofu cha Vatican siku zote kimeichukulia si kama nchi iliyo pembezoni mwa historia, bali kama ujumbe kwa ulimwengu. Kutokana na mtazamo huu, matumaini yetu ni makubwa kwamba ziara yako nchini mwetu itakuwa na mafanikio yote yanayotarajiwa, na itachangia kuimarisha umoja wa kitaifa uliotikiswa katika nchi hii ambayo imejaa majeraha kutokana na mashambulizi endelevu ya “Israel” dhidi ya watu wake na ardhi yake.
Sheikh Al-Khatib aliongeza kusema: Utamaduni wetu wa kiroho umejengwa juu ya undugu wa kibinadamu; nasi tunauchota kutoka katika misingi ya Uislamu ambayo haijali tofauti kati ya wanadamu, kama anavyosema Mtume wetu mtukufu Muhammad bin Abdullah (s.a.w.w):
“Hakuna ubora wa Mwarabu juu ya asiye Mwarabu isipokuwa kwa taqwa.”
Vilevile, tunauchukua kutoka katika fikra za mrithi wa Mtume huyo mtukufu, Amirul-Mu’minin Imam Ali bin Abi Talib (a.s), ambaye kwa maneno yake ya kibinadamu yenye maana pana sana, aliainisha hakika ya uhusiano kati ya wanadamu aliposema:
“Watu wako katika makundi mawili: ima ni ndugu yako katika dini au ni sawa na wewe katika umbile.”
Aliendelea kusema: Sisi tunajiona kuwa ni ndugu katika imani na sawa katika umbile, na hatuoni tofauti baina ya watoto wa binadamu isipokuwa kwa msingi wa taqwa. Tofauti ni sehemu ya maumbile ya wanadamu, na uhusiano baina ya tofauti hufuata mazungumzo, kufahamiana, kushirikiana katika wema na taqwa; na kuishi kwa amani kati ya wafuasi wa dini mbalimbali ndio kanuni na msingi. Na yale yanayotokea kwa jina la dini yakaitwa vita vya kutengenezwa, hayo hayaakisi ukweli wa dini; kwani dini kimsingi imejengwa juu ya heshima na hadhi ya mwanadamu.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Waislamu wa Kishia alisema pia: Sisi tunaamini juu ya umuhimu wa uwepo wa serikali, lakini kutokana na kutokuwepo kwake, tulilazimika kujilinda kwa kupinga uvamizi wa mkoloni aliyeshambulia ardhi yetu. Hatupendi kubeba silaha wala kuwatoa sadaka watoto wetu. Kwa kuzingatia hayo yote, tunalikabidhi suala la Lebanon mikononi mwenu, kwa kuzingatia uwezo wa kimataifa mlionao, kwa matumaini kwamba ulimwengu utaisaidia nchi yetu iondokane na misukosuko iliyojikusanya juu yake, na hasa uvamizi wa “Israel” na athari zake kwa taifa na watu wetu.
Maoni yako